Jumapili 12 Julai 2026 - 09:50
Rais wa Tano wa Indonesia: Imam Shahidi Hakuwa Kiongozi wa Iran Pekee, Bali Alama ya Mapambano na Uadilifu

Hawza/ Rais wa tano wa Indonesia amesema: "Kwa mtazamo wangu, shakhsia ya Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali Khamenei haikuwa tu ya kiongozi wa kisiasa au mwanazuoni wa kidini kutoka taifa la Iran anayejulikana kwa uzalendo wake mkubwa na kutokukubali kamwe kujisalimisha,mimi ninamuona kuwa ni mwendelezo wa mapambano yale ambayo baba yangu, Bung Karno, aliyianzisha."

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Megawati Sukarnoputri, Rais wa tano wa Jamhuri ya Indonesia na Mwenyekiti Mkuu wa Chama cha Democratic Party of Struggle (PDIP), ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Ayatullah Ali Khamenei, aliyekuwa Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ujumbe huo wa rambirambi ulitolewa kabla ya kufanyika kwa mazishi ya mwili wa Ayatullah Khamenei, na pia ulirushwa na moja ya vituo vya televisheni vya Iran.

Megawati amesema katika salamu zake za rambirambi kuwa; kufariki kwa Ayatullah Khamenei ni pigo kubwa, si kwa Iran pekee, bali pia kwa watu wengi wanaozithamini tunu za uadilifu na ubinadamu.

Alisema: "Kufariki kwa Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali Khamenei si msiba mkubwa kwa taifa la Iran pekee, bali pia kumetikisa nyoyo za watu wengi duniani wanaopenda uadilifu, haki ya mataifa kujitawala na misingi ya ubinadamu."

Ujumbe huo wa video wa rambirambi ulitumwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliopo Jakarta. Baadaye, moja ya vituo vya televisheni vya Iran vilivyokuwa vikirusha mubashara shughuli za mazishi ya Ayatullah Khamenei, viliurusha ujumbe huo.

Megawati pia alieleza kuwa; kwa mtazamo wake, Ayatullah Khamenei hakuwa tu kiongozi wa kisiasa au shakhsia ya kidini. Kwa mujibu wake, alikuwa mpambanaji mwenye roho imara na azma isiyotetereka.

Aliongeza: "Kwa mtazamo wangu, shakhsia ya Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali Khamenei haikuwa tu ya kiongozi wa kisiasa au mwanazuoni wa kidini kutoka taifa la Iran anayejulikana kwa uzalendo wake mkubwa na kutokukubali kamwe kujisalimisha. Mimi ninamuona kuwa ni mwendelezo wa mapambano yale ambayo baba yangu, Bung Karno, aliyianzisha."

Megawati pia alikumbuka mkutano wake na Ayatullah Khamenei wakati wa ziara yake rasmi mjini Tehran mwaka 2004, alipokuwa Rais wa Jamhuri ya Indonesia, na kusema kuwa kumbukumbu ya mkutano huo bado imebaki wazi kabisa akilini mwake.

Alisema: "Bado ninakumbuka kwa uwazi ziara yangu rasmi mjini Tehran mwaka 2004, nilipokuwa Rais wa Jamhuri ya Indonesia. Ilikuwa katika ziara hiyo ndipo nilipopata fursa ya kukutana naye ana kwa ana."

Aliendelea kusema: "Wakati huo nilihisi ndani yake haiba yenye nguvu sana pamoja na utulivu wa kina. Alikuwa mwanazuoni mpole lakini aliyesimama imara juu ya misingi yake, na wakati huo huo alikuwa mwanasiasa aliyekuwa na hisia na kujali mateso ya watu wake."

Megawati pia alikumbusha mtazamo chanya wa Ayatullah Khamenei kuhusu Pancasila na Roho ya Bandung, akisema kuwa; aliviona kama rejea muhimu katika kujenga dira ya Iran huru na yenye heshima. Alisema jambo hilo linaonyesha uhusiano wa kihistoria na wa karibu uliopo kati ya Indonesia na Iran.

Alisema: "Katika kuuenzi na kuuhifadhi ukumbusho wake, narudia tena kusisitiza uungaji mkono wangu kwa utatuzi wa migogoro kupitia amani, mazungumzo ya haki, kuheshimu sheria za kimataifa na misingi ya kibinadamu, badala ya kutumia vurugu na mashambulizi ya kijeshi ya upande mmoja."

Mwishoni mwa ujumbe wake, Megawati alimwombea Ayatullah Khamenei, familia yake, viongozi, maulamaa na taifa la Iran, huku akieleza matumaini yake kwamba Mwenyezi Mungu Atamjaalia makao bora kabisa.

Alisema: "Kwa familia kubwa ya marehemu, viongozi na maulamaa wa Iran, pamoja na wananchi wote wa Iran, ninawatakia dua zangu za dhati kabisa. Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mwingi wa Msamaha na Mwingi wa Rehema amrahisishie njia yake, azikubali juhudi zake zote, na amsamehe makosa yake yote."

Chanzo: Detik.com

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha